Lugha za Nairobi
Ramani hii inaonyesha walikotoka wahamiaji Waafrika huku jedwali likionyesha tarakwimu za makundi hayo jijini Nairobi. Jumuiya za wasemaji lugha kutoka nchi jirani za Kenya (Uganda, Tanzania, Somalia, Sudani Kusini, na Ethiopia) ni 75% ya idadi ya Waafrika waliohamia Nairobi. Aidha, jumuiya za watu kutoka DR Kongo, Kongo, Burundi na Rwanda ni asilimia 23%; Nigeria na Eritrea ni 3%, huku wale kutoka kusini mwa Afrika (Afrika Kusini, Zambia, na Zimbabwe) ni 1.6%.
Nchi za Afrika
(walimotoka wahamiaji wa Nairobi)
Afrika ya Kati
Burundi
Burundi ni nchi iliyoko Afrika ya kati inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Kongo), Rwanda, na Tanzania. Makabila makuu ni Wahutu, Watutsi, na Watwa. Lugha kuu ni Kirundi lakini watu wengi wanazumgumza lugha zingine. Warundi waliihama nchi yao kutokana na migogoro mingi ya kisiasa. Baadhi ya migogoro hiyo imejikita katika historia ya ukoloni na mizozo ya nchi zinazoizingira nchi hii ndogo kieneo.
Afrika ya Kati
DR Kongo
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi iliyoko Afrika ya kati. Inapakana na nchi za Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Rwanda, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda, na Zambia. Makabila makuu ni Wamongo, Waluba, Wakongo, na Wamangbetu-Azande. Makabila haya ni takribani asilimia arobaini na tano ya watu wote wa nchi. Lugha kuu ni Kilingala, Kingwana (lahaja ya Kiswahili), Kikongo, na Kishiluba. Tangu kupinduliwa na kuuawa kwa Waziri Mkuu Patrice Lumumba mapema miaka ya sitini, nchi hii kubwa na tajiri imekuwa na mizozo iliyosababisha wengi kuhama na kusambaza muziki na lugha zao kupitia bendi maarafu kama Mangelepa, Super Mazembe, n.k.
Afrika ya Kaskazini Mashariki
Eritirea
Eritirea ni nchi iliyoko Afrika ya Kaskazini Mashariki inayopakana na Jibuti, Ethiopia, na Sudani. Makabila makuu ni Watigrinya na Watigre ambayo yana asilimia hamsini na thelathini mtawalia ya idadi ya watu wa Eritrea. Lugha kuu ni Kitigrinya, Kiarabu, na Kiingereza. Watu wengi wa Eritrea walihama kwa sababu nchi ina serikali ya kijeshi inayosemekana kutotilia maanani sana haki za binadamu na kwa hivyo watu wameihama nchi.
Afrika Kaskazini Mashariki
Ethiopia
Ethiopia ni nchi iliyoko Afrika ya Kaskazini Mashariki inayopakana Jibuti, Eritirea, Kenya, Somalia, Sudani, na Sudani Kusini. Makabila Makuu ni Waoromo, Waamhara, Wasomali, Watigray, na Wasidama. Waoromo na Waamhara wanaunda idadi kubwa ya watu. Lugha rasmi ni Kiamhara lakini Kioromo ni lugha kuu ya jimbo la Oromiya.
Afrika ya Kati
Rwanda
Rwanda ni nchi iliyoko Afrika ya kati inayopakana na Tanzania, DR Congo, Burundi, na Uganda. Lugha kuu nchini Rwanda ni Kinyarwanda lakini Kiingereza na Kifaransa pia huzungumzwa. Rwanda ina makabila makuu matatu: Wahutu, Watutsi na Watwa (Imbuti wa Kongo). Takriban 94% ya watu wanazungumza Kinyarwanda nchini humo. Rwanda ilikuwa eneo la mauaji ya halaiki mwaka 1994. Hii ilisababisha uhamaji mkubwa. Wakimbizi walikwenda Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Afrika ya Mashariki
Somalia
Somalia ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki inayopakana na Ethiopia, Kenya, Jibuti, na bahari ya hindi. Wasomalia wana nasaba ya Kisomali, Kiarabu, na kibantu. Lugha kuu ni Kisomali na Kiarabu. Serikali ya Somalia haijatulia tangu Rais Said Barre ang'olewe mamlakini. Kutokuwa na serikali imara kwa muda kumesababisha mizozo ya kupigania uongozi na hatari za kiusalama. Makundi yenye mielekeo ya kigaidi yamewahangaisha wengi na kusababisha wengi kuwa wakimbizi.
Afrika ya Kaskazini Mashariki
Sudani Kusini
Sudan Kusini ni nchi iliyoko Afrika ya Kazskazini Mashariki inayopakana na Kenya, Sudani, Uganda, DR Kongo, Ethiopia, na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Sudani Kusini imekuwa na migogoro kuhusu udhibiti wa ardhi na Sudani na Kenya. Watu wa Sudani Kusini wanazungumza Kiingereza, Kiarabu, na lugha za kiasili kama vile Kidinka, Kinuer, Kibari, Kizande, na Kishilluk. Sudani Kusini ni kitovu cha lugha nyingi za Kinailoti. Nchi hii changa ilipata uhuru wake mwaka 2011. Wengi waliishi uhamishoni wakati wa vita dhidi ya Sudani na wakati wa mzozo baina ya Rais Silva Kiir na aliyekuwa makamu wake.
Afrika ya Mashariki
Tanzania
Tanzania ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki inayopakana na Burundi, DR Kongo, Kenya, Malawi, Mozambique, Rwanda, Uganda, na Zambia. Nchi ya Tanzania ni muungano wa Tanganyika bara na kisiwa cha Zanzibar. Kuna makabila mia moja na thelathini. Lugha kuu ni Kiswahili ingawa katika Zanzibar lugha ya pili ni Kiarabu. Tanzania ni mojawapo ya nchi kuu zinazowapokea wakimbizi wa Kiafrika.
Afrika ya Mashariki
Uganda
Uganda ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki inayopakana na DR Kongo, Rwanda, Tanzania, Kenya na Sudan Kusini. Uganda ina zaidi ya makabila sitini na matano ambayo yanazungumza lugha kutoka kwa vikundi vitatu kati ya vinne vya lugha kuu za Afrika. Tangu miaka ya 1970, maelfu ya Waganda waliihama nchi kwa sababu za kuepuka utawala wa mabavu Jenerali Idi Amin Dada, na vita vya kumng'oa Amin mamlakani. Wengi wakawa walimu tajika na wafanyibiashara jijini Nairobi na kwingeniko nchini Kenya.
Afrika ya Kusini
Afrika Kusini
Afrika Kusini ni nchi iliyoko kusini mwa Afrika inayopakana Botswana, Lesotho, Msumbiji, Namibia, eSwatini, na Zimbabwe. Watu wengi ni Waafrika weusi. Lugha kuu ni Kizulu, Kikhosa, Kisepedi, Kisetswana, Kiingereza, Kisotho, Kisonga, KiSwati, Kivenda, Kindebele na lugha nyingine. Kabla ya kupata uhuru mwaka 1994 Afrika Kusini ilikuwa chini ya serikali ya makaburu wachache walioendeleza serikali katili yenye sera za ubaguzi wa rangi. Hii ilisababisha Waafrika wengi weusi kukimbia kutoka nchi.
Afrika ya Kusini
Zambia
Zambia ni nchi iliyoko Afrika ya Kusini inayopakana na Angola, Botswana, DR Kongo, Malawi, Msumbiji, Namibia, Tanzania, na Zimbabwe. Makabila makuu ni Wabemba, Watonga, Wachewa, Walozi, na Wansenga. Lugha kuu za Zambia ni Kibemba, Kinyanja, na Kitonga. Kila lugha kuu ya Zambia ni ya kibantu.
Afrika ya Kusini
Zimbabwe
Zimbabwe ni nchi iliyoko Afrika ya Kusini inayopakana na Botswana, Msumbiji, Nchi ya Afrika Kusini, na Zambia. Makabila makuu ni Washona na Wandebele lakini kuna vikundi vingine pia. Kishona ni lugha kuu na Kindebele ni lugha ya pili. Kundi la wamisheni Waafrika kutoka Zimbabwe walihamia Nairobi kupitia nchi za Zambia na Tanzania. Wameishi Nairobi na vitongoji vyake tangu miaka ya sitini. Ingawa wanajulikana kama Washona wa Kenya, kundi hili linajumuisha lugha nyingi kutoka kusini mwa Afrika.
Afrika ya Kati
Kongo
Jamhuri ya Kongo ni nchi iliyoko Afrika ya kati Magharibi inayopakana na Angola, Kameruni, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Gabon. Makabila makuu ni Wakongo, Wateke, Wambochi, na Wasangha. Lugha kuu ni Kilingala, Kikongo, na Kifaransa. Ina watu wengi wanaoishi katika miji.
Afrika Magharibi
Nigeria
Nigeria ni nchi iliyoko Afrika ya Magharibi inayopakana na Benin, Kameruni, Chad, na Niger. Makabila makuu ni Wahausa, Wayoruba, Waigbo, na Wafulani. Nigeria ni nchi ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu katika Afrika. Lugha kuu ni Kihausa, Kiyoruba, Kiigbo, Kifulani, na zaidi ya lugha 500 za kiasili. Wahamiaji kutoka Nigeria wameongozeka miaka ya hivi karibuni.